Ziara ya Rais Samia Nchini China na Matunda Yake kwa Tanzania.

Ziara ya Rais Samia Nchini China na Matunda Yake kwa Tanzania.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amehudhuria mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC), unaofanyika jijini Beijing China kuanzia tarehe 02 hadi 06 Septemba 2024.

Mkutano huo unaowakutanisha viongozi toka barani Afrika na Taifa hilo la pili kwa uchumi duniani umehudhuriwa na Marais/Wakuu wa nchi kutoka takribani nchi zote za Afrika

USHIRIKIANO WA KIMKAKATI.

Akizungumza na vyombo vya habari, Balozi wa Tanzania nchini China, Khamis Omar ameeleza kuwa FOCAC mwaka huu ni mwendelezo wa ilipoishia FOCAC yam waka uliopita 2021. Balozi Omar anasema kuwa anatarajia matokeo chanya takribani manne kutoka katika mkutano huo ambapo ameainisha sekta zitazoguswa. Maeneo hayo ni pamoja na:

Maendeleo ya miundombinu (hasa reli ya TAZARA),

Uzalishaji (Kuanzia kipindi cha miaka ya 1960 hadi sasa, imekuwa ikiunga mkono Tanzania katika maeneo ya uzalishaji, kilimo, na viwanda)

Ushirikiano katika sekta binafsi za kibiashara


MTAZAMO WA WASOMI/WANAZUONI

Mchambuzi mwandamizi wa uchumi, Profesa Haji Semboja anasema hivi sasa China imepiga hatua kubwa katika teknolojia, hivyo kuimarisha uhusiano nao kupitia jukwaa hilo kunaweza kufanikisha mipango wa maendeleo. Anasisitiza kuw ni muhimu kwa Tanzania kushiriki, kwani endapo ikikaa nyuma inakuwa haipo kwenye mipango yao hivyo hata manufaa yanaweza yasipatikane.

Mwanazuoni wa sera za Afrika, Profesa Peter Kagwanja anasema FOCAC imekuwa jukwaa muhimu la ushirikiano wa kiuchumi kati ya China na Afrika, likichangia ukuaji wa uchumi, maendeleo ya miundombinu, na kuboresha ustawi wa jamii barani Afrika.Kwa kipindi cha miaka 24 iliyopita, kupitia FOCAC na BRI, China imeelekeza zaidi ya dola bilioni 200 kusaidia maendeleo ya bara la Afrika

KILICHOIPELEKA TANZANIA

Taarifa iliyotolewa Agosti 31, 2024 na Serikali imeeleza kuwa  kuwa Rais Samia anatarajiwa kuwasilisha miradi minne kwa Serikali ya China kwa lengo la kupatiwa fedha za mkopo nafuu na msaada ya utekelezaji wake. Miradi ambayo Waziri alisema itakayowasilishwa na Rais Samia kwenye mkutano huo ni:

Ujenzi wa mtandao wa mawasiliano vijijini awamu ya pili,

Ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa kilovoti 400 awamu ya pili na ya tatu,

Ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi (Veta) awamu ya pili na,

Ujenzi wa barabara za Zanzibar zenye urefu wa kilomita 277.

Tanzania inatarajia kuwasilisha miradi mbalimbali, ikiwemo mipya na ile ambayo haikuweza kutekelezwa kwenye mpango uliopita wa FOCAC kwa sababu mbalimbali, ili iweze kupatiwa fedha za mkopo nafuu na msaada na kutekelezwa chini ya mpango kazi wa FOCAC mwaka 2025-2027

RAIS SAMIA NA MPANGO WA KUVUTIA WAWEKEZAJI ZAIDI TANZANIA.

Akiwa nchini China Rais Samia amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Xi Jinping katika ukumbi wa The Great Hall of the People.

Katika mazungumzo yao, Rais Dkt. Samia amesema uhusiano wa nchi hizo mbili ni muhimu na ametoa wito wa kuendelea kudumisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali pamoja na kuendeleza ushirikiano katika Mpango wa Kuendeleza Miundombinu na Kukuza Uwekezaji (Belt and Road Initiative) ili kuleta manufaa yanayoonekana kwa wananchi.

Rais Dkt. Samia ametoa wito kwa sekta binafsi nchini China kuwekeza Tanzania katika uzalishaji wa vyanzo vya nishati mbadala na miundombinu ya usambazaji.

Katika mkutano huo, Rais Xi alisema kuwa China iko tayari kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati yake na Tanzania ili kuleta manufaa zaidi kwa nchi zote mbili na kuendeleza uhusiano wa kihistoria ulioasisiwa na waasisi na kurithiwa na vizazi vya sasa.

Baada ya mazungumzo yao, Rais Dkt. Samia, Rais Xi Jinping na Rais wa Zambia Mhe. Hakainde Hichilema walishuhudia uwekaji saini wa Hati ya Makubaliano (MOU) baina ya Tanzania, Zambia na China kuhusu uboreshaji wa reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Baraza la Mashauriano ya Kisiasa la Watu wa China (CPPCC), Mhe. Wang Huning.

Vilevile, akiwa nchini China, Rais Samia atafanya mazungumzo na kampuni za China ambazo zipo tayari kufanya uwekezaji mkubwa na kufungua ofisi zao hapa Tanzania. Hatua hii ni muhimu sana katika kuhamasisha uwekezaji zaidi nchini Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published.